WATU WAWILI WAFARIKI KATIKA MATUKIO TOFAUTI

Tuesday, January 15, 2013 | comments

WATU WAWILI wamefariki dunia Mkoani Manyara katika matukio tofauti likiwemo la mmoja kufa maji wakati mwengine akiokotwa huku akiwa ameharibiwa sehemu zake za siri kutokana na kubakwa na kulawitiwa.

Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Bw. Akili Mpwapwa alisema tukio moja lilitokea Januari 10 majira ya saa 11.30 jioni katika maeneo ya Mrara Mjini Babati mwanamke mmoja aliokotwa kwenye korongo akiwa amefariki. Alimtaja marehemu kuwa ni Mwanaisha Iddi (25) mkulima na mkazi wa kijiji cha Gichameda, ambaye alikutwa amefariki huku akiwa amechuchumaa na sehemu zake za siri kuharibiwa vibaya kutokana na kuingiliwa kwa nguvu.

Kamanda alieleza kuwa kufuatia uchunguzi wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa mtu mmoja amekamatwa kutokana na kuhusishwa na tukio hilo ambapo ilidaiwa kuwa mtuhumiwa na marehemu walikuwa na mahusiano ya kimapenzi.

Aidha alimtaja mtuhumiwa kwa jina la John Mathayo Barani (35) mkulima na mkazi wa kijiji cha Gichameda ambapo alielezwa kuwa wana watoto wawili na siku ya tukio mtuhumiwa alimpigia simu marehemu na walikutana katika eneo hilo. Kamanda Mpwapwa aliendelea kueleza kwamba wakati mtuhumiwa alipokuwa akiendelea kumfanyia marehemu kitendo cha kumlawiti alimkaba koo mpaka akafariki na kuongeza kuwa chanzo cha tukio hilo hakijafahamika.

Wakati huohuo tukio jingine lilitokea Januari 13 majira ya asubuhi katika kijiji cha Qash, Wilayani Babati ambapo mwanafunzi mmoja wa darasa la tatu katika shule ya msingi Qash alifariki dunia wakati akiwa anaogelea katika bwawa lililochimwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Na Alex Mchomvu.

Kaya 20 zahofiwa kukosa makazi.

Thursday, January 10, 2013 | comments

ZAIDI ya kaya 20 katika Kijiji cha Mbiligili kitongoji cha Mateteni wilayani Kilosa zimekosa mahali pa kuishi baada ya kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa inayonyesha katika milima ya Kiteteto mkoani Manyara na Ukaguru mkoani Morogoro.

Baadhi ya wanakijiji waliozungumza na Tanzania Daima jana walisema mvua hiyo ilianza kunyesha kidogo kidogo Jan 7 majira ya saa 10:00 jioni na baadaye kuongezeka na kunyesha kwa zaidi ya saa mbili.

Walisema kutokana na wingi wa mvua hiyo kuna uwezekano wa kupata mafuriko kutokana na maeneo hayo kuwa na historia ya kutiririsha maji mengi ambayo yanawaathiri kila mwaka na kupoteza mali mbalimbali.

“Unajua ilipoanza kila mtu hakutegemea kama ingekuwa mvua kubwa kwa kuwa ilianza kidogo kidogo lakini ilipochukua muda mwingi kunyesha nikawa na hofu nikijua lazima mafuriko yatukumbe,” alisema Husina Rajabu.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Iddi Mangilile, alisema maji hayo yalimwagwa na mto wa msimu unaosadikiwa kukusanya maji kutoka katika milima ya Kiteto na Ukaguruni kupitia mto Mkundi ambao umehama njia yake.

Na Alex Mchomvu

MAJIVU YATUMIKA KUPANGA UZAZI NA UTOAJI MIMBA MBEYA

Wednesday, January 9, 2013 | comments

Mkurugenzi Mkuu wa Hosptal ya Rufaa jijini Mbeya Eleuter Samky


LICHA ya Serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutoa elimu ya kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango kote nchini, baadhi ya wanawake katika wilaya ya Mbeya Vijijini na Jiji la Mbeya wamekuwa wakitumia majivu kama njia ya kupanga uzazi na kutoa mimba zisizotarajiwa.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii katika mji wa Mbalizi Mbeya Vijijini na kata ya Manga na Foresti Jijini Mbeya umebaini kuwa wanaoongoza kwa kutumia njia hiyo ni pamoja na wake za watu na wahudumu wa Bar.

Wanawake waliohojiwa wakiwemo wawili kati yao ambao wakawa na mahusiano na mwandishi wa makala haya ili kukamilisha uchunguzi, walisema kuwa majivu hayo wanakunywa kikombe kimoja kila baada ya kumaliza kufanya tendo la ndoa na wanaume ambao wana mahusiano nao ya kimapenzi na wengine waume zao. ‘’Majivu unatakiwa unywe ndani ya masaa 12 baada ya kutoka kufanya tendo la ndoa ili mimba isitunge’’ anasema Mama Angel mkazi wa eneo la Mama John ambaye ni mke wa mtu.

Mama Angel anakiri kuwa amewahi kutoa mimba kwa njia za kisasa ambayo haikuwa mimba ya mumewe na alipoambiwa kuwa kuna njia zingine za kujikinga ikiwemo kunywa majivu baada ya tendo la ndoa ameendelea kutumia njia hiyo kwa miaka mitatu sasa. ‘’Kule hospitali nilitundikiwa maji ya uchungu ambayo yanaongeza njia na ndani ya masaa matatu mimba ikatoka’’ anasema Mama Angel bila kutaja hospitali aliyotolea mimba. Uchunguzi huo uliofanywa mwezi Octoba na Novemba 2012, umebaini kuwa kwa sasa wanawake wengi hawapendi kutumia njia za uzazi wa mpango wa kisasa mfano Sindano, vipandikizi na vidonge kwa madai kuwa huduma hizo zina madhara. Wanawake 43 waliohojiwa wakiwemo wake za watu 13 walisema kuwa madhara waliyoyapata baada ya kutumia njia za uzazi wa mpango wa kisasa ni pamoja na kupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa.

Baadhi walisema kuwa wanaogopa kufanyiwa upasuaji (kusafishwa) kunakotokana na uvimbe unaosadikika kutokea baada ya kutumia kwa muda mrefu huduma hizo za kisasa hasa vidonge maarufu kama majira. ‘’Tarehe za Hedhi hubadilika na kutoeleweka baada ya kutumia dawa hizo za uzazi wa mpango wa kisasa zikiwemo sindano na vidonge’’ anasema Naomi Haule ambaye ni mhudumu wa Bar.

Wengine ambao waliomba hifadhi ya majina yao, wanasema mbali na kutumia majivu kama njia ya uzazi wa mpango kuzuia mimba na utoaji mimba, baadhi yao wanatumia kisamvu, Vidonge vya uzazi wa mpango maarufu kama (Majira) na majani ya mti unaojulikana kwa jina la Songwa kutoa mimba zisizotarajiwa. ‘’Wake za watu wanaopata mimba ambazo si za waume wao, wafanyabiashara na wahudumu wa Bar siyo siri tunaongoza katika kutumia njia hizi na utoaji mimba kwa njia za kienyeji’’ anasema Rehema Mwakitalu akiwa na wenzake eneo la Mwanjelwa ambaye pia ni muhudumu wa Bar.

Walipoulizwa kuwa kwanini wasitumie njia za kisasa katika utoaji mimba walisema kuwa kikwazo ni gharama za utoaji mimba kwa njia za kisasa ambapo mwanamke mwenye mimba ya mwezi mmoja hutozwa Shilingi 40,000 ili asaidiwe kutoa mimba hiyo. Walizitaja hospitali ambazo zinahusika kutoa mimba hizo kwa siri kuwa ni pamoja na hospitali ya wazazi Meta na zahanati zingine za madaktari binafsi zilizopo eneo la Nzovwe, Mama John na Uyole. Aidha mbali na hospitali hizo, wanawake hao walisema kuwa pia kuna waganga na wakunga wa jadi wanaowasaidia kutoa mimba hizo ambazo wanadai kuwa hazikutarajiwa na kwamba wakunga hao wapo eneo la Mapelele wilaya ya Mbeya na Iwambi Jijini Mbeya. Kuhusu maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi wanasema; ‘’

Ni bora kupata ukimwi kuliko mimba kwasababu ukipata ukimwi unajulikana baada ya muda sana na unapata dawa za kurefusha maisha lakini mimba ukipata huwezi kuendelea na starehe na ukijifungua unalazimika kulea mtoto kwa muda mrefu huku na wanaume wengi hawaeleweki kwenye matunzo’’ wanasema wanawake hao.

Wanawake wahudumu wa Bar walipoulizwa kuwa kwanini wanatumia zaidi majivu kama njia ya uzazi wa Mpango na utoaji Mimba walisema kuwa baadhi ya wanaume huwa hawapendi kutumia mipira (Condom) wakati wa kujamiiana hivyo baada ya tendo la ndoa wanalazimika kutumia njia hiyo kama moja ya njia rahisi ya kuzuia mimba kutotunga. Walipoulizwa kama wanajua madhara ya kutumia huduma ya majivu na kisamvu kwa muda mrefu kama huduma ya uzazi wa mpango na utoaji mimba walisema kuwa hofu yao ni kwamba wanaweza kupata kansa au kutozaa tena. ‘’Ili kuepukana na kupata madhara ya kansa yanayoweza kutokana na majivu, huwa mtu akinywa basi siku hiyo anatakiwa kunywa maji kwa wingi ili kupunguza kemikali zitokanazo na majivu’’ anasema Asha Juma.

Anasema yeye ni Mama wa watoto watatu na tangu amepata mtoto wake wa kwanza mwaka 1998 amekuwa akitumia majivu kila baada ya tendo la ndoa. Na kwamba alipojaribisha kutumia vidonge alisumbuliwa na nyonga na kukosa hamu ya tendo la ndoa hatimaye akaenda kusafishwa na alipojaribisha sindano pia alipata madhara ya kukosa hamu ya tendo la ndoa ambapo mpaka sasa anatumia Majivu kama njia salama kwake ya uzazi wa mpango Baadhi ya madaktari waliohojiwa kwa sharti la kutoandika majina yao gazetini wamekiri kuhusika na biashara ya utoaji mimba kwa njia za kisasa na kuzitaja njia wanazotumia. ‘’Wenzetu kuna sheria za utotaji mimba lakini ajabu hapa Tanzania tunakataza wakati watu wengi wanatoa mimba tena hasa wake za watu na njia ambazo wengi tunazitumia kwa usalama zaidi ni kuwatundikia Drip za maji ya uchungu na vidonge vya uchungu vinavyoongeza njia kwa mwanamke’’wanasema madaktari hao kwa nyakati tofauti.

Siku wanazotumia zaidi ni siku za Jumapili ambapo wanasema kuwa baada ya kumaliza utoaji huo wa mimba wanawake hao wanatoka wakiwa salama na kuwapatia dawa za kutuliza maumivu na kuwashawishi kula vyakula na vinywaji vya kuongeza damu. Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, katika sayansi ya akili watu wanaojamiiana huwa wanatumia kinga mara ya kwanza na ya pili baada ya kuanza mahusiano na huwa hawatumii tena kinga baada ya kukutana mara ya tatu na nne na kuendelea.

Sanjari na hayo imebainika kuwa wauguzi wengi huwa hawatumii njia za kisasa za uzazi wa mpango licha ya kuendelea kuwashawishi wananchi wengine kutumia njia hizo kwa madai kuwa vidonge hivyo huwa wakimeza haviyeyuki. ‘’Sisi wengi hatutumii kwasababu kuna madhara makubwa ukitumia kwa muda mrefu ambapo ukitaka kuzaa unalazimika kwenda kusafishwa kizazi na vidonge hivyo haviyeyuki na inatia hofu kuwa ukikwanguliwa unaweza usizae tena’’ walisema baadhi ya wauguzi wa hospitali za Ifisi Mbalizi na hospitali ya wazazi Meta kwa sharti la kutotaja majina yao.

Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Mbeya Prisca Butuyuyu, anasema kuwa mila na desturi ni tatizo katika utumiaji sahihi wa uzazi wa mpango na kwamba katika wilaya ya Mbeya Vijijini mwaka 2011 vilitokea vizazi hai 38 kati ya 100,000 na vifo 113. Kwa upande wa Jiji la Mbeya mwaka 2011 anasema vizazi vilikuwa 109 kati ya 100,000 na vifo vilikuwa 363 ambapo katika uzazi huo hospitali ya wazazi meta ndiyo inahusika zaidi na inahudumia wanawake pia wanaotoka nje ya Jiji la Mbeya.

Nchi gani Afrika si tegemezi?

| comments

MWAKA 1951 nchi ya kwanza Afrika ilipata uhuru na kufikia mwaka 1966, nchi karibu zote zilipata uhuru isipokuwa sita tu. Kwa maana hiyo, si vibaya kusema Bara la Afrika kwa wastani liko kwenye miaka ya 50 ya uhuru wake kutoka kwa wakoloni.

Kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru Afrika kinakwenda sambamba na miaka 50 ya watu wa rangi hasa weusi nchini Marekani, kuwa na haki kamili za kiraia (civil rights) baada ya kupitishwa sheria ya haki za kiraia (civil rights act), mwaka 1964 na ile ya haki ya kupiga kura (voting rights act) mwaka 1965.

Sheria hizi mbili ziliondosha kabisa sheria za kibaguzi zilizojulikana kama Jim Crow; sheria zilizokuwa zikitenganisha wazungu na jamii nyingine hasa weusi, kwa kila nyanja za maisha yao mfano shule za weupe na weusi, sehemu za kukaa kwenye mabasi (weusi walitakiwa kukaa nyuma na kukaa mbele ilikuwa kosa kisheria) na pia katika makazi.

Sheria za kibaguzi za Jim Crow ndiyo zilizopingwa na Martin Luther King, hadi kuawa kwake mwaka 1968, King alitaka watu wote bila kujali rangi wawe na haki sawa nchini Marekani, lakini Marcus Garvey na Malcom X walikuwa na maoni tofauti.

Ingawa Malcom X alikuwa akibadili mtazamo kulingana na mwenendo wa wakati, yeye na Marcus Garvey kwa nyakati tofauti walitaka weusi wawe na nchi yao, kwa maana taifa la weusi iwe kurudishwa Afrika au kupewa sehemu ya Marekani waanzishe taifa la weusi.

Madhumuni ya Marcus Garvey na Malcom X kutaka sheria za kibaguzi ni kuonyesha kwamba watu weusi wanavipawa au akili kama Wazungu.

Waliamini kabisa kwamba weusi wakiwa na taifa lao, wataweza kuwa na misingi mizuri ya kidemokrasia, kujitawala, kufanya biashara na mambo mengine mengi tu yanayohusu maisha ya mwanadamu.

Marcus Garey alizaliwa mwaka 1887 nchini Jamaica na kufariki mwaka 1940 jijini London, Uingereza. Aliendeleza harakati za kudai haki za weusi kutoka kwa weusi waliomtangulia kama Prince Hall, Martin Delany na Edward W. Blyden kwa kujikita zaidi kwenye falsafa ya Pan-Africanism (umajumui wa Afrika); itikadi na vuguvugu kuhimiza umoja wa watu weusi duniani.

Aliongoza harakati zake za ukombozi wa weusi kwa kutia hamasa ya weusi popote duniani kurudi barani Afrika liliko chimbuko lao.

Pia alihimiza uwezeshaji wa weusi kiuchumi kwa vitendo, baada ya kuhimiza weusi kuanzisha kampuni ya meli ya weusi iliyoitwa Black Star Line na gazeti la kila wiki lililojulikana kama Negro World lililopigwa marufuku na wakoloni kuingizwa katika makoloni yao Afrika.

Ni katika gazeti hilo la kila wiki la Negro World, Marcus Garvey aliweza kuandika na kuchapisha makala kuhimiza juu ya umoja wa watu weusi popote pale duniani.

Moja ya makala aliyoandika kwenye Negro World juu ya umoja wa weusi ni ile iliyokuwa na kichwa cha habari “African Fundamentalism”, moja ya nukuu kutoka kwenye makala hiyo ni “Our union must know no clime, boundary, or nationality; let us hold together under all climes and in every country…”, kwa tafsiri isiyo rasmi; “Umoja wetu usiangalie pande gani ya dunia, mipaka au utaifa bali tufungamane kutoka pande zote za dunia na katika kila nchi.”

Makala nyingine alizoandika ni kama “Society and The Selfish Exploiter”, hii ni makala iliyohusu unyonyaji na kuwaita watu wanaodhulumu wanyonge kuwa wahalifu zaidi ya wauaji.

Vilevile katika harakati za kupinga ukoloni uliokuwa ukiendelea Afrika, Marcus Garvey alitoa hotuba ya kusisimua kwa weusi waliojumuika kwenye ukumbi wa Liberty (Liberty hall), New York mwaka 1921 na kuipa kichwa; “Africa For The Africans”, nitatoa baadhi ya nukuu kutoka kwenye hotuba hiyo sambamba na tafsiri isiyo rasmi:

“Say! Africa for the Africans,
Like America for the Americans:
This the rallying cry for a nation,
Be it in peace or revolution.
Blacks are men, no longer cringing fools;
They demand a place, not like weak tools;
But among the world of nations great
They demand a free self-governing state”.

“Sema! Afrika kwa Waafrika.
Kama Marekani kwa Wamarekani:
Hiki ni kilio cha kudai taifa,
Iwe ni kwa amani au kwa mapinduzi.
Weusi ni binadamu, sio tena wajinga;
Wanadai sehemu, wao sio dhana dhaifu;
Bali kati ya mojawapo ya mataifa duniani,
Wanadai taifa huru linalojitawala”

Ndugu zangu, hayo ni maneno ya Marcus Garvey miaka 30 kabla nchi ya kwanza Afrika ipate uhuru na miaka 45 kabla karibu kila nchi Afrika ipate uhuru, isipokuwa nchi sita tu.

Miaka 11 baada ya kifo chake nchi ya kwanza Afrika ilipata uhuru na miaka 26 baada ya kifo chake, nchi karibu zote zilipata uhuru. Hivyo harakati zake japo za kutaka weusi kuachiwa Afrika zilikamilika akiwa tayari ameiaga dunia, kwa bahati mbaya pia alikuwa amefariki kabla ya kukanyaga ardhi ya Afrika.

Kwa upande wa Malcom X, yeye mpaka kuawa kwake mwaka 1965, karibu nchi nyingi za Afrika zilikuwa zimepata uhuru.

Aliuawa takribani miezi sita kabla ya Wamarekani weusi kuwa na haki sawa za kiraia kwa kupitisha sheria ya mwisho ya haki ya kupiga kura (voting rights act). Kama nilivyosema mwanzoni, Malcom X alikuwa akibadilika kiasi kwenye mitizamo yake kadiri muda ulivyokuwa unakwenda lakini bado msimamo wake ulikuwa wa kuhimiza utengano wa weusi na wazungu, kwa maana na weusi kuwa na taifa lao.

Aliendelea kudai kwamba kwa muda wa zaidi ya miaka 400 ya mateso ya weusi nchini Marekani, basi Marekani igharimie usafiri wa watu weusi kurudi Afrika au wapewe ardhi sehemu ya Marekani waanzishe taifa la weusi na waweze kuonyesha uwezo wao kwamba ni binadamu kama wengine, wanaweza kujitawala, kufanya biashara na mambo mengine.

Pia aliendelea kupinga juu ya Marekani kuingilia mambo ya nchi za Afrika na hii inajionyesha pale baada ya kuawa Rais Kennedy, wa Marekani wakati huo siku iliyofuata kiongozi wake mkuu wa kundi la Kiislam la Nation of Islam, alimsihi kutozungumzia kabisa mambo yanayohusu Rais Kennedy kesho yako kwenye mkutano.

Lakini alipoulizwa swali na mwandishi kuhusu kuawa kwa Rais Kennedy, baada ya kumaliza hotuba yake, Malcom hakuonyesha kushangaa kwani alisema hayo ni malipo juu ya machafuko yanayosababishwa na Marekani duniani kote, na mnukuu hapa “Being an old farm boy myself, chickens coming home to roost never did make me sad, they have always made me glad.” Aliendelea kudai kwamba Rais Kennedy ndiye aliagiza kuuawa kwa Waziri Mkuu wa Congo, Patrick Lumumba. Malcom X alisimamishwa kufanya kazi za kundi hilo la Nation of Islam kwa siku 90, lakini hakurudi tena na alianzisha kundi lake na kuuawa mwaka mmoja baadaye.

Wote Marcus Garvey na Malcom X walikuwa na shauku ya kuona Waafrika wakijitawala na kuonyesha dunia kwamba weusi wanauwezo mkubwa wa kujitawala na ni binadamu kama binadamu wengine.

Kwa sasa ni miaka zaidi ya 50 tangu Bara la Afrika lianze kujitawala na naweza kusema itikadi za hawa magwiji kutaka Waafrika wajitawale zimejaribiwa ila swali je, tumeweza kujitawala kwa misingi bora ya demokrasia, utawala bora, kuondoa baa la njaa kila mara na kuacha utegemezi?

Ni nchi gani Afrika ambayo sio tegemezi? Hata zile zenye rasilimali zaidi ya nchi ya Italia, kama Tanzania bado zinategemea misaada kutoka kwa wakoloni (siku hizi mnawaita wafadhili).

Swali ambalo wengi tutakuwa tunajihuliza ni; je, kweli juhudi zote zilizofanywa na kundi hili la wapigania haki za watu weusi wakiwa na lengo la kuhahakikisha Mwafrika anapoachiwa ajitawale ataonyesha uwezo wake, zimefanikiwa?

Malengo yao ya kutaka mtu mweusi awe na taifa lake huru aonyeshe vipawa vyake vyote alivyopewa na Mwenyezi Mungu, yametimia? Bara la Afrika linatawaliwa na weusi kwa zaidi ya miaka 50, hivi kweli tumeweza kuonyesha uwezo wa mweusi kuudhihirishia Ulimwengu wa wazungu kwamba ndiyo tumeweza? Au ni kauli mbiu tu za kila mara kwamba tumedhubutu, tumeweza, tunasonga mbele?

Je, leo Marcus Garvey na Malcom X wakifufuka, wataweza kuwabeza wazungu kwamba si mnaona tuliwaambia mkiacha tujitawale tutaonyesha kwamba sisi ni binadamu kama nyie na uwezo tunao, na tangu mtuache weusi tuwe na nchi zetu huru haya ndiyo maendeleo tuliyonayo.

Au wazungu ndiyo watakaowabeza akina Garvey na Malcom kwamba tulijua weusi hawawezi kujitawala, kwa miaka zaidi ya hamsini tuwape Bara lenu bado mnatutegemea kwa kila kitu, mmeshindwa kuwalisha watu wenu, mnagombana wenyewe kwa wenyewe.

Nikifikiria Bara la Afrika lilipo kwa sasa, ni kwamba ndoto zote za hao magwiji wa haki za weusi hazijatimia kwa maana ya kuonyesha uwezo na kuweka heshima kwa mweusi katika nchi huru anayoitawala.

Bara la Afrika halijaweza kuonyesha thamani halisi ya Mwafrika na kuonyesha uwezo wa Mwafrika, huo ndiyo ukweli.

Haya ndiyo yaliyokuwa malengo ya akina Garvey na Malcom na weusi wengine waliokuwa utumwani, kujenga heshima ya mtu mweusi kwa kuonyesha uwezo katika nchi huru anayoitawala. Mwonekano uko wazi, bado taifa ni tegemezi.

Swala hili si kwa Marcus Garvey na Malcom X au jamii ya Wamarekani weusi tu waliokuwa na mtizamo kama wao bali ni kwa Waafrika ndani ya Bara la Afrika, waliokuwa na mitizamo kama hiyo, mfano, Kwame Nkrumah wa Ghana, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Thomas Sankara wa Burkina Faso na Samora Machel wa Msumbiji, mlolongo ni mrefu wa Waafrika wenzetu waliojitoa kwa ajili ya Bara letu lakini hawako nasi kuona mwelekeo wa Bara hili na kuzidi kupotea kwa heshima ya mtu mweusi waliyokuwa wakiipigania na kuijenga, enzi zao.

Tunabaki tu na maswali kama wakifufuka iwe kwa wale waliopata uhuru kwa amani au mapinduzi pengine wakapewa nafasi ya mdahalo kama waliokuwa nao kipindi wakidai uhuru kutoka kwa wakoloni ni hoja hizi zipi wataingia nazo kutetea uhuru wa Mwafrika baada ya miaka 50? Je ni hoja kwamba binadamu wote ni sawa?

Ndio, inawezekana tuko sawa, watasema tuliwapa nchi zenu mzitawale, na je, uwezo wa kujitawala kwa ufanisi tumeuonyesha au bado ni mtindo ule ule wa kuwalaumu wazungu?

Kila mwaka tarehe ya kuadhimishwa uhuru inapofika kwa kila nchi Afrika, mbwembwe ni nyingi, sambamba na sherehe za gharama.

Sina hakika kama viongozi wetu huwashirikisha wananchi kutafakari madhumuni ya wapigania huru wetu na hadhi ya Mwaafrika ulimwenguni. Au ni mtindo ule wa kunywa mvinyo na kuthamini kuwapo kwao madarakani, kufurahia fursa za kukutana na marais au mawaziri wa nchi za kizungu na kupigiwa mizinga na kuandaliwa tafrija ughaibuni katika Ikulu za wenzetu. Je, hayo ndiyo yaliyokuwa madhumuni ya kudai uhuru?

Kwamba mtu mweusi anapigiwa mizinga ya urais Marekani na Uingereza, inawezekana rais huyo kutoka Afrika akaona hiyo ndiyo heshima na ukombozi kwa Mwafrika.

Ni hapo rais kutoka Afrika anapoulizwa kwa nini nchi yako ni masikini anajibu kwamba hata yeye haelewi ni kwa nini. Sasa kama rais haelewi na anakaa madarakani kwa miaka 10, inawezekana katika miaka 50 ya uhuru basi toa miaka 10, jibu utapata miaka 40 ya uhuru, na kama mtangulizi wake alikuwa haelewi basi toa tena miaka 10 unapata miaka 30 ya uhuru.

Kwa mtindo huu, kama watawala wetu hawaelewi kwa nini Bara letu bado ni masikini, ukitoa miaka yao katika miaka 50 ya uhuru wa Afrika inawezekana Bara letu likawa bado haliko huru; linaitaji wakombozi wapya wanaotambua kwa nini hili Bara ni masikini mbali na kujaaliwa rasilimali lukuki, wakombozi watakaoweza kutimiza malengo ya wapigania uhuru na haki za mtu mweusi popote pale dunia.

Ninatambua kwamba wako watu weusi wengi walioonyesha uwezo katika masuala mbalimbali kama uongozi, michezo, taaluma, lakini wachache hao hawawezi kuchukuliwa kama mfano kuonyesha kwamba weusi tumethubutu na tumeweza.

Heshima ya Mwafrika iko kwenye kuliendeleza Bara la Afrika, kukomesha majanga ya njaa ya kila mara na vita ya wenyewe, pia kuonyesha ukomavu wa demokrasia.

Hata hao wachache kwenye medani ya michezo wameonyesha uwezo wao nje ya Bara la Afrika na hii inaonyesha kwamba kama Bara tumeshindwa kuwa na mipango madhubuti kujiendeleza kimichezo, na hili si michezo tu hata kwenye taaluma.

Kwa upande wa uongozi wale waliothubutu kuonyesha uwezo wa kiuongozi kama Thomas Sankara wa Burkina Faso waliishia kuawa na Waafrika wenzao.

Je, kweli tumeweza kuonyesha kwamba Afrika huru imefikia au inaelekea kufikia malengo ya kutaka kujitawala kwa miaka hamsini ya uhuru wake na kuweka heshima ya mtu mweusi popote pale duniani?

Watoto Watafunwa na Funza Korogwe Vijijini

Sunday, January 6, 2013 | comments

Baadhi ya watoto wanaoshambuliwa na ugonjwa wa funza. Kuanzia mtoto wa pili kutoka kulia ni miongoni mwa familia zinazoshambuliwa na ugonjwa wa funza eneo la Kibaoni Korogwe Vijijini.
Hata hivyo si watoto wa familia zote wamekubwa na ugonjwa huo, wapo ambao wanaangaliwa kwa karibu na familia zao kama wanavyoonekana baadhi ya watoto katika picha hii, ambao wamesalimika. Funza Korogwe Vijijini BAADHI ya watoto wanaokosa uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi au walezi wao wamekubwa na ugonjwa wa kushambuliwa na funza kwa kiasi kikubwa miguuni na mikononi hali iliyosababisha kuharibika kwa miguu yao na mikono kiasi kikubwa. Idadi kubwa ya watoto walioathiriwa na wadudu hao wameonekana katika eneo la Kibaoni Korogwe vijijini, ambapo baadhi walipohojiwa na Thehabari walizitupia lawama familia zao kwa kutowaangalia kwa karibu kiasi cha kushambuliwa na funza. Kassim (si jina lake sahihi) anasema nyumbani kwao watoto wote wameshambuliwa na funza kuanzia miguuni hadi mikononi hali ambayo imewanyima kuwa huru katika kujumuika na wenzao. “Wadudu hawa wanawasha na kuleta maumivu makali kiasi ambacho hushindwa hata kujumuika nawenzako…huwa najaribu wapunguza na kumsaidia mdogo wangu pia lakini wanatuzidi ni wengi,” anasema mtoto huyo. Hata hivyo mbali na maumivu na kuwashwa mfululizo, mikono ya kijana huyu imeshambuliwa vibaya na funza kiasi kinachomnyima uhuru wa kuitumia mikono vizuri kushikia vitu anuai kutokana na maumivu. Ardhi ya kibaoni ni ya udogo mwekundu wenye vumbi hasa kipindi cha kiangazi. Baadhi ya watu wanasema wadudu aina ya funza wanaoshambulia binadamu ustawi zaidi katika mazingira machafu na yenye vumbi kiasi kikubwa. Watoto na hata watu wanaoshambuliwa na wadudu hao wanaishi katika mazingira kama hayo.

Baadhi ya familiya ya Vijijini Tanzania.

| comments

                                                  Naomba Tujiulize Kuhusu Maisha haya,Jamani.


                                                               Hebuona tena hii.
 
Support : Designer | Ibrahim Haruna | +255716606570
Copyright © 2011. SAUTI YA VIJIJINI - All Rights Reserved
Template Created by TheDynamite Published by TRJA
Proudly powered by Nativebase Company