ZAIDI ya kaya 20 katika Kijiji cha Mbiligili kitongoji cha Mateteni wilayani Kilosa zimekosa mahali pa kuishi baada ya kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa inayonyesha katika milima ya Kiteteto mkoani Manyara na Ukaguru mkoani Morogoro.
Baadhi ya wanakijiji waliozungumza na Tanzania Daima jana walisema mvua hiyo ilianza kunyesha kidogo kidogo Jan 7 majira ya saa 10:00 jioni na baadaye kuongezeka na kunyesha kwa zaidi ya saa mbili.
Walisema kutokana na wingi wa mvua hiyo kuna uwezekano wa kupata mafuriko kutokana na maeneo hayo kuwa na historia ya kutiririsha maji mengi ambayo yanawaathiri kila mwaka na kupoteza mali mbalimbali.
“Unajua ilipoanza kila mtu hakutegemea kama ingekuwa mvua kubwa kwa kuwa ilianza kidogo kidogo lakini ilipochukua muda mwingi kunyesha nikawa na hofu nikijua lazima mafuriko yatukumbe,” alisema Husina Rajabu.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Iddi Mangilile, alisema maji hayo yalimwagwa na mto wa msimu unaosadikiwa kukusanya maji kutoka katika milima ya Kiteto na Ukaguruni kupitia mto Mkundi ambao umehama njia yake.
Na Alex Mchomvu
Post a Comment