Nchi gani Afrika si tegemezi?

Wednesday, January 9, 2013 | comments

MWAKA 1951 nchi ya kwanza Afrika ilipata uhuru na kufikia mwaka 1966, nchi karibu zote zilipata uhuru isipokuwa sita tu. Kwa maana hiyo, si vibaya kusema Bara la Afrika kwa wastani liko kwenye miaka ya 50 ya uhuru wake kutoka kwa wakoloni.

Kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru Afrika kinakwenda sambamba na miaka 50 ya watu wa rangi hasa weusi nchini Marekani, kuwa na haki kamili za kiraia (civil rights) baada ya kupitishwa sheria ya haki za kiraia (civil rights act), mwaka 1964 na ile ya haki ya kupiga kura (voting rights act) mwaka 1965.

Sheria hizi mbili ziliondosha kabisa sheria za kibaguzi zilizojulikana kama Jim Crow; sheria zilizokuwa zikitenganisha wazungu na jamii nyingine hasa weusi, kwa kila nyanja za maisha yao mfano shule za weupe na weusi, sehemu za kukaa kwenye mabasi (weusi walitakiwa kukaa nyuma na kukaa mbele ilikuwa kosa kisheria) na pia katika makazi.

Sheria za kibaguzi za Jim Crow ndiyo zilizopingwa na Martin Luther King, hadi kuawa kwake mwaka 1968, King alitaka watu wote bila kujali rangi wawe na haki sawa nchini Marekani, lakini Marcus Garvey na Malcom X walikuwa na maoni tofauti.

Ingawa Malcom X alikuwa akibadili mtazamo kulingana na mwenendo wa wakati, yeye na Marcus Garvey kwa nyakati tofauti walitaka weusi wawe na nchi yao, kwa maana taifa la weusi iwe kurudishwa Afrika au kupewa sehemu ya Marekani waanzishe taifa la weusi.

Madhumuni ya Marcus Garvey na Malcom X kutaka sheria za kibaguzi ni kuonyesha kwamba watu weusi wanavipawa au akili kama Wazungu.

Waliamini kabisa kwamba weusi wakiwa na taifa lao, wataweza kuwa na misingi mizuri ya kidemokrasia, kujitawala, kufanya biashara na mambo mengine mengi tu yanayohusu maisha ya mwanadamu.

Marcus Garey alizaliwa mwaka 1887 nchini Jamaica na kufariki mwaka 1940 jijini London, Uingereza. Aliendeleza harakati za kudai haki za weusi kutoka kwa weusi waliomtangulia kama Prince Hall, Martin Delany na Edward W. Blyden kwa kujikita zaidi kwenye falsafa ya Pan-Africanism (umajumui wa Afrika); itikadi na vuguvugu kuhimiza umoja wa watu weusi duniani.

Aliongoza harakati zake za ukombozi wa weusi kwa kutia hamasa ya weusi popote duniani kurudi barani Afrika liliko chimbuko lao.

Pia alihimiza uwezeshaji wa weusi kiuchumi kwa vitendo, baada ya kuhimiza weusi kuanzisha kampuni ya meli ya weusi iliyoitwa Black Star Line na gazeti la kila wiki lililojulikana kama Negro World lililopigwa marufuku na wakoloni kuingizwa katika makoloni yao Afrika.

Ni katika gazeti hilo la kila wiki la Negro World, Marcus Garvey aliweza kuandika na kuchapisha makala kuhimiza juu ya umoja wa watu weusi popote pale duniani.

Moja ya makala aliyoandika kwenye Negro World juu ya umoja wa weusi ni ile iliyokuwa na kichwa cha habari “African Fundamentalism”, moja ya nukuu kutoka kwenye makala hiyo ni “Our union must know no clime, boundary, or nationality; let us hold together under all climes and in every country…”, kwa tafsiri isiyo rasmi; “Umoja wetu usiangalie pande gani ya dunia, mipaka au utaifa bali tufungamane kutoka pande zote za dunia na katika kila nchi.”

Makala nyingine alizoandika ni kama “Society and The Selfish Exploiter”, hii ni makala iliyohusu unyonyaji na kuwaita watu wanaodhulumu wanyonge kuwa wahalifu zaidi ya wauaji.

Vilevile katika harakati za kupinga ukoloni uliokuwa ukiendelea Afrika, Marcus Garvey alitoa hotuba ya kusisimua kwa weusi waliojumuika kwenye ukumbi wa Liberty (Liberty hall), New York mwaka 1921 na kuipa kichwa; “Africa For The Africans”, nitatoa baadhi ya nukuu kutoka kwenye hotuba hiyo sambamba na tafsiri isiyo rasmi:

“Say! Africa for the Africans,
Like America for the Americans:
This the rallying cry for a nation,
Be it in peace or revolution.
Blacks are men, no longer cringing fools;
They demand a place, not like weak tools;
But among the world of nations great
They demand a free self-governing state”.

“Sema! Afrika kwa Waafrika.
Kama Marekani kwa Wamarekani:
Hiki ni kilio cha kudai taifa,
Iwe ni kwa amani au kwa mapinduzi.
Weusi ni binadamu, sio tena wajinga;
Wanadai sehemu, wao sio dhana dhaifu;
Bali kati ya mojawapo ya mataifa duniani,
Wanadai taifa huru linalojitawala”

Ndugu zangu, hayo ni maneno ya Marcus Garvey miaka 30 kabla nchi ya kwanza Afrika ipate uhuru na miaka 45 kabla karibu kila nchi Afrika ipate uhuru, isipokuwa nchi sita tu.

Miaka 11 baada ya kifo chake nchi ya kwanza Afrika ilipata uhuru na miaka 26 baada ya kifo chake, nchi karibu zote zilipata uhuru. Hivyo harakati zake japo za kutaka weusi kuachiwa Afrika zilikamilika akiwa tayari ameiaga dunia, kwa bahati mbaya pia alikuwa amefariki kabla ya kukanyaga ardhi ya Afrika.

Kwa upande wa Malcom X, yeye mpaka kuawa kwake mwaka 1965, karibu nchi nyingi za Afrika zilikuwa zimepata uhuru.

Aliuawa takribani miezi sita kabla ya Wamarekani weusi kuwa na haki sawa za kiraia kwa kupitisha sheria ya mwisho ya haki ya kupiga kura (voting rights act). Kama nilivyosema mwanzoni, Malcom X alikuwa akibadilika kiasi kwenye mitizamo yake kadiri muda ulivyokuwa unakwenda lakini bado msimamo wake ulikuwa wa kuhimiza utengano wa weusi na wazungu, kwa maana na weusi kuwa na taifa lao.

Aliendelea kudai kwamba kwa muda wa zaidi ya miaka 400 ya mateso ya weusi nchini Marekani, basi Marekani igharimie usafiri wa watu weusi kurudi Afrika au wapewe ardhi sehemu ya Marekani waanzishe taifa la weusi na waweze kuonyesha uwezo wao kwamba ni binadamu kama wengine, wanaweza kujitawala, kufanya biashara na mambo mengine.

Pia aliendelea kupinga juu ya Marekani kuingilia mambo ya nchi za Afrika na hii inajionyesha pale baada ya kuawa Rais Kennedy, wa Marekani wakati huo siku iliyofuata kiongozi wake mkuu wa kundi la Kiislam la Nation of Islam, alimsihi kutozungumzia kabisa mambo yanayohusu Rais Kennedy kesho yako kwenye mkutano.

Lakini alipoulizwa swali na mwandishi kuhusu kuawa kwa Rais Kennedy, baada ya kumaliza hotuba yake, Malcom hakuonyesha kushangaa kwani alisema hayo ni malipo juu ya machafuko yanayosababishwa na Marekani duniani kote, na mnukuu hapa “Being an old farm boy myself, chickens coming home to roost never did make me sad, they have always made me glad.” Aliendelea kudai kwamba Rais Kennedy ndiye aliagiza kuuawa kwa Waziri Mkuu wa Congo, Patrick Lumumba. Malcom X alisimamishwa kufanya kazi za kundi hilo la Nation of Islam kwa siku 90, lakini hakurudi tena na alianzisha kundi lake na kuuawa mwaka mmoja baadaye.

Wote Marcus Garvey na Malcom X walikuwa na shauku ya kuona Waafrika wakijitawala na kuonyesha dunia kwamba weusi wanauwezo mkubwa wa kujitawala na ni binadamu kama binadamu wengine.

Kwa sasa ni miaka zaidi ya 50 tangu Bara la Afrika lianze kujitawala na naweza kusema itikadi za hawa magwiji kutaka Waafrika wajitawale zimejaribiwa ila swali je, tumeweza kujitawala kwa misingi bora ya demokrasia, utawala bora, kuondoa baa la njaa kila mara na kuacha utegemezi?

Ni nchi gani Afrika ambayo sio tegemezi? Hata zile zenye rasilimali zaidi ya nchi ya Italia, kama Tanzania bado zinategemea misaada kutoka kwa wakoloni (siku hizi mnawaita wafadhili).

Swali ambalo wengi tutakuwa tunajihuliza ni; je, kweli juhudi zote zilizofanywa na kundi hili la wapigania haki za watu weusi wakiwa na lengo la kuhahakikisha Mwafrika anapoachiwa ajitawale ataonyesha uwezo wake, zimefanikiwa?

Malengo yao ya kutaka mtu mweusi awe na taifa lake huru aonyeshe vipawa vyake vyote alivyopewa na Mwenyezi Mungu, yametimia? Bara la Afrika linatawaliwa na weusi kwa zaidi ya miaka 50, hivi kweli tumeweza kuonyesha uwezo wa mweusi kuudhihirishia Ulimwengu wa wazungu kwamba ndiyo tumeweza? Au ni kauli mbiu tu za kila mara kwamba tumedhubutu, tumeweza, tunasonga mbele?

Je, leo Marcus Garvey na Malcom X wakifufuka, wataweza kuwabeza wazungu kwamba si mnaona tuliwaambia mkiacha tujitawale tutaonyesha kwamba sisi ni binadamu kama nyie na uwezo tunao, na tangu mtuache weusi tuwe na nchi zetu huru haya ndiyo maendeleo tuliyonayo.

Au wazungu ndiyo watakaowabeza akina Garvey na Malcom kwamba tulijua weusi hawawezi kujitawala, kwa miaka zaidi ya hamsini tuwape Bara lenu bado mnatutegemea kwa kila kitu, mmeshindwa kuwalisha watu wenu, mnagombana wenyewe kwa wenyewe.

Nikifikiria Bara la Afrika lilipo kwa sasa, ni kwamba ndoto zote za hao magwiji wa haki za weusi hazijatimia kwa maana ya kuonyesha uwezo na kuweka heshima kwa mweusi katika nchi huru anayoitawala.

Bara la Afrika halijaweza kuonyesha thamani halisi ya Mwafrika na kuonyesha uwezo wa Mwafrika, huo ndiyo ukweli.

Haya ndiyo yaliyokuwa malengo ya akina Garvey na Malcom na weusi wengine waliokuwa utumwani, kujenga heshima ya mtu mweusi kwa kuonyesha uwezo katika nchi huru anayoitawala. Mwonekano uko wazi, bado taifa ni tegemezi.

Swala hili si kwa Marcus Garvey na Malcom X au jamii ya Wamarekani weusi tu waliokuwa na mtizamo kama wao bali ni kwa Waafrika ndani ya Bara la Afrika, waliokuwa na mitizamo kama hiyo, mfano, Kwame Nkrumah wa Ghana, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Thomas Sankara wa Burkina Faso na Samora Machel wa Msumbiji, mlolongo ni mrefu wa Waafrika wenzetu waliojitoa kwa ajili ya Bara letu lakini hawako nasi kuona mwelekeo wa Bara hili na kuzidi kupotea kwa heshima ya mtu mweusi waliyokuwa wakiipigania na kuijenga, enzi zao.

Tunabaki tu na maswali kama wakifufuka iwe kwa wale waliopata uhuru kwa amani au mapinduzi pengine wakapewa nafasi ya mdahalo kama waliokuwa nao kipindi wakidai uhuru kutoka kwa wakoloni ni hoja hizi zipi wataingia nazo kutetea uhuru wa Mwafrika baada ya miaka 50? Je ni hoja kwamba binadamu wote ni sawa?

Ndio, inawezekana tuko sawa, watasema tuliwapa nchi zenu mzitawale, na je, uwezo wa kujitawala kwa ufanisi tumeuonyesha au bado ni mtindo ule ule wa kuwalaumu wazungu?

Kila mwaka tarehe ya kuadhimishwa uhuru inapofika kwa kila nchi Afrika, mbwembwe ni nyingi, sambamba na sherehe za gharama.

Sina hakika kama viongozi wetu huwashirikisha wananchi kutafakari madhumuni ya wapigania huru wetu na hadhi ya Mwaafrika ulimwenguni. Au ni mtindo ule wa kunywa mvinyo na kuthamini kuwapo kwao madarakani, kufurahia fursa za kukutana na marais au mawaziri wa nchi za kizungu na kupigiwa mizinga na kuandaliwa tafrija ughaibuni katika Ikulu za wenzetu. Je, hayo ndiyo yaliyokuwa madhumuni ya kudai uhuru?

Kwamba mtu mweusi anapigiwa mizinga ya urais Marekani na Uingereza, inawezekana rais huyo kutoka Afrika akaona hiyo ndiyo heshima na ukombozi kwa Mwafrika.

Ni hapo rais kutoka Afrika anapoulizwa kwa nini nchi yako ni masikini anajibu kwamba hata yeye haelewi ni kwa nini. Sasa kama rais haelewi na anakaa madarakani kwa miaka 10, inawezekana katika miaka 50 ya uhuru basi toa miaka 10, jibu utapata miaka 40 ya uhuru, na kama mtangulizi wake alikuwa haelewi basi toa tena miaka 10 unapata miaka 30 ya uhuru.

Kwa mtindo huu, kama watawala wetu hawaelewi kwa nini Bara letu bado ni masikini, ukitoa miaka yao katika miaka 50 ya uhuru wa Afrika inawezekana Bara letu likawa bado haliko huru; linaitaji wakombozi wapya wanaotambua kwa nini hili Bara ni masikini mbali na kujaaliwa rasilimali lukuki, wakombozi watakaoweza kutimiza malengo ya wapigania uhuru na haki za mtu mweusi popote pale dunia.

Ninatambua kwamba wako watu weusi wengi walioonyesha uwezo katika masuala mbalimbali kama uongozi, michezo, taaluma, lakini wachache hao hawawezi kuchukuliwa kama mfano kuonyesha kwamba weusi tumethubutu na tumeweza.

Heshima ya Mwafrika iko kwenye kuliendeleza Bara la Afrika, kukomesha majanga ya njaa ya kila mara na vita ya wenyewe, pia kuonyesha ukomavu wa demokrasia.

Hata hao wachache kwenye medani ya michezo wameonyesha uwezo wao nje ya Bara la Afrika na hii inaonyesha kwamba kama Bara tumeshindwa kuwa na mipango madhubuti kujiendeleza kimichezo, na hili si michezo tu hata kwenye taaluma.

Kwa upande wa uongozi wale waliothubutu kuonyesha uwezo wa kiuongozi kama Thomas Sankara wa Burkina Faso waliishia kuawa na Waafrika wenzao.

Je, kweli tumeweza kuonyesha kwamba Afrika huru imefikia au inaelekea kufikia malengo ya kutaka kujitawala kwa miaka hamsini ya uhuru wake na kuweka heshima ya mtu mweusi popote pale duniani?
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Designer | Ibrahim Haruna | +255716606570
Copyright © 2011. SAUTI YA VIJIJINI - All Rights Reserved
Template Created by TheDynamite Published by TRJA
Proudly powered by Nativebase Company