HALMASHAURI ya Wilaya ya Rombo imeanza mipango ya kutumia ufugaji wa nyuki kukabiliana na tembo waharibifu ambao mara kadhaa huvamia baadhi ya makazi ya wananchi maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kufanya uharibifu wa mazao pamoja na kuua au kujeruhi wakazi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wilayani hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Judethadeus Mboya alisema tayari halmashauri hiyo imetengeneza mizinga ya nyuki ambayo imesambazwa maeneo kadhaa ili kukabiliana na tembo waharibifu eneo hilo.
“Unajua nimetembea mbuga mbili za Kenya ikiwemo Tsavo ambazo tumepakana nazo eneo hili sehemu ambayo tembo hutokea huko na kuvamia maeneo yetu, sehemu hizi wao wamedhibiti uvamizi wa tembo…wamefuga nyuki wengi sana na maeneo mengine wametumia hadi teknolojia kuwazuia tembo kuvamia makazi ya raia hivyo hawapati madhara kama yetu,” alisema Mboya akifanya mazungumzo na gazeti hili ofisini.
Alisema kwa sasa tayari wametengeneza mizinga 50 ya nyuki na kuifunga ukanda wa chini wa vijiji kama Chala, Ibukoni, Ngoyoni na maeneo mengine ambayo tembo huyatumia kama njia kipindi cha uvamizi na kwa sasa mizinga mingine 100 ya nyuki inaandaliwa kuenezwa maeneo mengine kukabiliana na tembo hao hatari.
Alisema viongozi wa halmashauri hiyo pia wametoa elimu kwa wanakijiji maeneo husika ya kuhamasisha uvugaji nyuki katika vikundi ikiwa ni jitihada za kukabiliana na tembo hao waharibifu ambao idadi kubwa hutokea nchi jirani ya Kenya na kufanya uharibifu pamoja na kutishia maisha ya wanavijiji upande wa Tanzania.
Aidha kiongozi huyo alisema tembo hao mbali na kufanya uhalibifu mkubwa wa mazao ya wanavijijini kipindi cha uvamizi wakati mwingine wamekuwa wakiuwa raia jambo ambalo ni hatari zaidi kiusalama.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebaini uvamizi wa wanyama hao umekuwa kero kwa maeneo mbalimbali ya vijiji vya wilaya hiyo, kiasi ambacho unatishia shughuli za maendeleo ya wananchi kama kilimo pamoja na maendeleo ya elimu kwa ujumla.
Akizungumzia hali ya uvamizi wa tembo na athari za elimu, Mwalimu wa Taaluma Shule ya Sekondari Tanya, Shuma Himidiel alisema miezi ambayo tembo huanza kufanya uvamizi huingilia ratiba za masomo na mara kadhaa kusimama kutokana na hofu ya wanafunzi na usalama wao hasa wanapotoka na kuja shuleni.
“Kimsingi wanyama hawa wanapoanza usumbufu kijiji kizima huwa na heka heka na wakati mwingine hata wanafunzi wanashindwa kuja shule kuhofia maisha yao…hata wazazi huwazuia watoto wao kutoka hadi hali ya hatari inaporejea kuwa ya kawaida.
Akifafanua zaidi mwalimu Himidiel alisema mara ya mwisho tembo kufanya uvamizi katika Kijiji cha Tanya waliua mtu mmoja walipokuwa wakidhibitiwa na askari wa wanyamapori eneo hilo.
Na Alex.